Jamhuri Kihwelo 'Julio' na Michael Richard Wambura wanaongombea nafasi za makamu wa Rais na Makamu Rais mtawalia, wakirejesha fomu za ugombea makao makuu ya klabu hiyo.
MCHEZAJI na kocha wa zamani wa Simba SC, Jamhuri Mussa Kihwelo ‘Julio’ amechukua na kurudisha fomu ya kugombea umakamu wa Rais wa klabu hiyo.
Julio alishangaza watu pale alipolipia fomu za ugombea kwa kutoa noti mbili za pesa za kimarekani zenye thamani ya dola 100 kila moja kama ada ya fomu hiyo.
Aidha Julio amesema yeye anaifahamu Simba zaidi ya robo tatu ya viongozi waliopo ndani ya klabu hiyo kwa sasa na akadai kisheria yeye bado ni kocha wa klabu hiyo kwani kufukuzwa kwao hakukufuata katiba ya klabu hiyo.
Akaongeza kwamba yeye ni kocha pekee ambaye amekuwa akiitumikia klabu hiyo pale inapokuwa na matatizo ya kifedha kwani makocha wengine huwa hawakubali kufanya kazi bure, lakini Ila hali inapokaa sawa huwa anafukuzwa kwa kuambiwa hana elimu ya kutosha kuifundisha timu hiyo.
Julio alikuwa sambamba na mgombea mwingine Michael Richard Wambura anayegombea nafasi ya Urais wa klabu hiyo.
Wambura amesema anataka kuiongoza klabu hiyo kwa sababu kwa muda mrefu imeongozwa na watu wasio sahihi na kuifanya ishindwe kuishi kulingana na ukubwa wa jina lake.