Akizungumza na East Africa Radio, Katibu mkuu wa TFF Mwesigwa Celestine amesema, kocha ameshawasilisha Programu yake na wanaifanyia kazi kwa ajili ya maandalizi ya mechi hiyo inayotarajiwa kuchezwa Septemba tano mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Mwesigwa amesema, baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Kagame, Kocha anatarajiwa kutaja kikosi chake kitakachovaana na Nigeria katika michuano hiyo.
Kwa upande wa kutafuta kocha mwingine iwapo muda wa kocha wa sasa utamalizika, Mwesigwa amesema wanaelewa hakuna nchi iliyowahi kuchukua kombe la dunia ikiwa na kocha mgeni lakini wanaelewa umuhimu wa kuwa na kocha mgeni ili kuelewa na mazingira husika lakini suala la kutafuta kocha kuna mambo mengi yanayoangaliwa.
Mwesigwa amesema, muda wa kuwaangalia makocha wa sasa utakapokwisha ndiyo watajua ni nani anafaa na kwa sasa wana maombi mengi sana ya makocha mbalimbali lakini wakati ukifika watajua ni kocha yupi anafaa kwa ajili ya kukinoa kikosi cha Timu ya Taifa, Taifa Stars.