Tuesday , 16th Dec , 2014

Shirikisho la Soka nchini TFF limesema baada ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili jana usiku kwa vilabu vya Ligi Daraja la Kwanza, la Pili na Ligi Kuu, limepokea hati za uhamisho ITC za wachezaji nane wa kimataifa.

Mchezaji wa Yanga Emerson De Oliveira Neves Roque

Akizungumza jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Boniface Wambura amesema kuwa katika hati hizo, Sita zimekwisha hakikiwa na kuvifikia vilabu vilivyowasajili wachezaji hao wa hapa nchini ambao ni Mchezaji Serge Paschal wawa raia wa Ivory Coast aliyeombewa ITC na klabu ya Azam akitokea El Marreikh ya Sudan, Kpah Sean Sherman akitokea timu ya Ardhi Liberia akiwa ameombewa na Klabu ya Yanga.

Na wengine ni Meshack Abel aliyetokea KCB ya Nchini Kenya akiombewa ITC na Polisi Morogoro, Abdulhalim Humud Gaucho aliyeombewa ITC na Coastal Union akitokea Sofapaka ya nchini Kenya, Brayan Majwega aliyeombewa ITC na Azam FC akitokea timu ya KCC ya Uganda, Daniel Sserunkuma aliyeombewa ITC na Klabu ya Simba akitokea Gor Mahia ya nchini Kenya na Simon Sserunkuma akitokea Victoria University ya nchini Uganda akiwa ameombewa na Klabu ya Simba.

Wambura amesema wachezaji ambao maombi ya ITC zao yameshatumwa na wanasubiri muda wowote kutumwa ili kuweza kuvitumikia vilabu walivyosajiliwa ni Emerson De Oliveira Neves Roque aliyeombewa na Klabu ya Yanga akitokea Klabu ya Bonsucesso FC ya Nchini Brazil na Juko Murshid aliyeombewa na Klabu ya Simba akitokea Klabu ya Victoria University ya nchini Uganda.

Wambura amesema usajili huo unatakiwa kuzingatia sheria zilizowekwa ambapo kila klabu inatakiwa kusajili idadi ya wachezaji isiyopungua 18 na wasiozidi 30 ambapo baada ya kukamilika usajili kwa vilabu hivyo usajili huo utathibitishwa na kamati ya sheria na hadhi za Wachezaji wa TFF.