Tuesday , 9th Feb , 2016

Mlinzi wa kati na nahodha msaidizi wa timu ya Mtibwa Sugar, Salim Mbonde amesema hawatishiki na pengo la pointi kumi lilipo kati yao na Yanga katika msimamo wa ligi zaidi ya kuweka nia katika mbio za ubingwa hadi mwisho wa msimu ili kujua hatma yao.

Mbonde amesema msimu huu ni mgumu na ushindani ni wa hali ya juu lakini pointi 10 sio nyingi sana kwani hata wao nao hawashindi mechi zote kwahiyo wana imani bado wanaweza wakashinda mechi nyingine na wao wakapoteza.

Mtibwa ilianza msimu kwa nguvu kiasi cha kuonekana kama wangeweza kutoa ushindani katika mbio za ubingwa msimu huu lakini mambo yamewageukia na sasa wako nafasi ya 4 wakiwa na pointi zao 33.

Baada ya sare ya kufungana 1-1 na Ndanda SC siku ya Jumapili katika uwanja wa Nangwanda, Mtwara mabingwa hao mara mbili wa zamani hawatakuwa na mechi wiki hii kwa kuwa waliopaswa kuwa wapinzani wao Yanga SC watakuwa katika michezo ya klabu bingwa Afrika.