Sunday , 14th Oct , 2018

Timu ya taifa ya soka ya Kenya ‘Harambee Stars’ imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ethiopia na kuongoza kundi lake katika harakati za kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika AFCON mwakani nchini Cameroon.

Timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars

Harambee Stars iliyokuwa nyumbani mbele ya mashabiki wake waliojaa katika uwanja wa Kasarani, imeichapa Ethiopia baada ya kutoka sare katika mchezo wa mapema wiki hii, ugenini nchini Ethiopia.

Mabao ya Kenya yamefungwa na Michael Olunga katika dakika ya 23, Eric Johana Omondi katika dakila ya 28  na Victor Wanyama aliyefunga kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 67 ya mchezo.

Ushindi huo unaifanya Harambee Stars kufikisha alama saba baada ya kushuka dimbani michezo minne na kuongoza kundi lake, ikilingana na Uganda ambayo inaongoza kundi lake la ‘L’ kwa alama saba baada ya kushuka dimbani michezo mitatu mpaka sasa.

Kwa upande wa timu zingine za Afrika Mashariki, timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inaburuza mkia mpaka sasa katika kundi lake baada ya kushuka dimbani  michezo mitatu, ikikubali kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Cape Verde Oktoba 12.

Rwanda inaburuza mkia katika kundi lake la H ikiwa haina alama hata moja baada ya kufungwa mechi zote tatu mpaka sasa, huku Burundi ikiwa katika nafasi ya pili kwa alama tano katika kundi C.