Wednesday , 7th Nov , 2018

Chama cha soka nchini Uingereza (FA) kimeweka wazi mpango wake wa kukata rufaa juu ya uamzi wa mamlaka ya nidhamu wa kumwondolea hatia kocha wa klabu ya Manchester United, Mourinho.

Kocha wa Man United, Jose Mourinho

FA ilimshtaki Mourinho kwa tuhuma za kunaswa na kamera akitamka maneno ya matusi baada ya mchezo wa Manchester United dhidi ya Newcastle United, Oktoba 6, mchezo uliomalizika kwa United kushinda mabao 3-2 ikitokea nyuma baada ya kufungwa mabao 2-0.

Jalada la Mourinho lilfikishwa kwenye kamati ya nidhamu na maadili ili kujadili matamshi yake ambayo hayakusikika kwa sauti lakini wataalam wa lugha za ishara wanaamini Mourinho alitoa lugha ya matusi.

Baada ya kupitia mashtaka hayo (Independent Regulatory Commission) ilimkuta bila hatia kocha huyo raia wa Ureno hivyo kumwacha huru kitu ambacho FA inasema sio haki na itakata rufaa.

Video mbalimbali zilimwonesha Mourinho akitembea huku akirusha mkono wa kulia na mdomo ukiwa na ishara ya kutoa maneno baada ya timu yake kufanikiwa kutoka kufungwa mabao 2-0 kipindi cha kwanza na kushinda 3-2 katika mchezo huo.