Monday , 26th May , 2014

Chama cha cricket nchini Tanzania TCA kimetangaza mpango wa kuwaandalia ligi ndogo ya vijana wachezaji wa timu ya Taifa ili kuwapima uwezo kabla ya kwenda Zambia.

Wanamichezo vijana wa Cricket Tanzania.

Timu ya taifa ya vijana ya umri chini ya miaka 19 ya Tanzania ya mchezo wa Cricket inataraji kuingia kambi ya pamoja mapema mwezi Juni mwaka huu kujiwinda na michuano ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 19 daraja la pili michuano itakayofanyika Lusaka Zambia kuanzia juma la kwanza la mwezi wa nane, mwaka huu

Kocha wa timu hiyo Hamis Abdalah amesema wamelazimika kuingia kambini mapema ili kujiandaa vizuri kwakuwa mashindano hayo yatatoa wawakilishi wa mashindano ya dunia.

Aidha Hamis amesema walikua waanze maandalizi ya kambi ya pamoja kabla ya Juni lakini hali haikuwa hivyo hali ambayo imetokana na wachezaji wengi wa timu hiyo kuwa ni wanafunzi walio masomoni katika sehemu tofauti hapa nchini.

Amesema kuwa kikubwa ni kwamba chama kina wafuatilia kwa ukaribu wachezaji hao na wanaendelea kujifua huko waliko na baada ya kufunga shule wote watakusanyika jijini Dar es salaam kwa ajili ya kambi ya pamoja kuelekea katika michuano hiyo ya Afrika Division 2 kuwania tiketi ya kucheza kombe la dunia.