Mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani ikiwa ni muendelezo wa Michuano ya Ligi kuu soka Tanzania bara iliyoanza kutumia vumbi Septemba 26 mwaka jana.
Akizungumza leo, Ofisa Habari wa Coastal Union, Oscar Assenga amesema kuwa baada ya kumalizika mechi yao na JKT Ruvu, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mkenya James Nandwa akishirikiana na Mkurugenzi wa benchi la Ufundi Mohamed Kampira na Kocha wa Makipa Mfaume Athumani walikwisha kuyafanyia kazi mapungufu yaliyopelekea kupoteza mchezo huo.
Assenga amesema kuwa sasa baada ya kazi kubwa iliyofanywa na makocha hao kikosi hicho kipo kamili kuweza kuwavaa maafande wa Jeshi la Polisi kutoka mkoani Morogoro ili kuweza kuhakikisha wanabakiza pointi tatu muhimu.
Amesema kuwa licha ya kuhakikisha wanapata matokeo mazuri lakini wachezaji wanaounda kikosi hicho wamepania kuonesha kandanda safi ili kuweza kuwapa burudani wapenzi na mashabiki wa soka mkoani hapa.
Coastal Union iliyopo nafasi ya Tano kwenye msimamo wa Ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara imepania kufanya vizuri katika michezo yake iliyosalia kwenye mzunguko wa kwanza ili kuweza kupaa kileleni mwa ligi hiyo.