Akizungumza na East Africa Radio, Dada wa Marehemu, Wakuru Ndayenda amesema, Christopher alianza kusumbuliwa na TB miezi mitatu iliyopita na kuamua kuanza matibabu ya ugonjwa huo lakini baadaye alipatwa na ugonjwa wa kuchanganyikiwa na alipopimwa tena aligundulika na fangasi ya koo ambayo ilisambaa mpaka kichwani.
Ndayenda amesema, Christopher alizidiwa na magonjwa hayo Februari 11 ambapo alipelekwa hospitali ya Mirembe Februari 12 na ndipo alipokutwa na mauti leo asubuhi.
Christopher Alex Massawe ameacha watoto wawili ambapo anatarajiwa kuzikwa siku ya Jumanne makaburi ya Chinangali West mjini Dodoma.
Chama cha kandanda mkoa wa Dar es salaam DRFA,kimeeleza kusikitishwa kwake na kifo cha mchezaji kiungo wa zamani wa klabu ya simba na timu ya taifa-Taifa Stars,Christopher Alex maarufu kama Masawe,kilichotokea leo (februari 22 mwaka huu),katika Hospitali ya Mirembe Dodoma.
Mwenyekiti wa DRFA,Almas Kasongo,amemuelezea marehemu Christopher kuwa ni mchezaji aliyevuma enzi za uhai wake na kuiletea heshima kubwa klabu yake ya Simba na Taifa Kwa ujumla,pale walipofanikiwa kuisukumiza nje ya michuano ya afrika klabu ya Zamalek na kuivua ubingwa miamba hiyo ya soka ya kaskazini mwaka 2003.
Kiungo huyo aliyeanza kuvuma katika miaka ya 2000,amefariki dunia kutokana na kusumbuliwa kwa muda mrefu na ugonjwa wa kifua kikuu (TB).
Marehemu Christopher Alex, alizaliwa Septemba 12 mwaka 1975, na kupata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Uhuru na kumaliza katika shule ya Chamwino huko Dodoma mwaka 1993, na alianza kucheza mpira kwenye timu ya Daraja la nne Chamwino UTD na baadaye daraja la tatu akiwa na kikosi cha Aston Villa nayo ya Dodoma.
Mwaka 1999-2001 ameitumikia klabu ya CDA ya Dodoma,kabla ya kutimkia klabu ya Reli mwaka 2002 na baadaye kujiunga na wekundu wa msimbazi Simba,Marehemu ameacha mtoto mmoja aitwaye Alex.
Kasongo, kwa niaba ya kamati ya utendaji ya DRFA,wametoa ubani wa shilingi laki mbili (200,000/=) kwa familia ya marehemu, na kuwataka mashabiki wa soka na watanzania kwa ujumla kuungana pamoja katika kuifariji familia hiyo kwenye kipindi hiki kigumu cha majonzi.