Saturday , 14th May , 2016

Pamoja na kuonekana kuwa na msimu mbaya sana mwaka huu ikiwa chini ya kocha Mreno Jose Mourinho na kuokolewa na kocha wa muda Guuz Hiddink matajiri wa London, Chelsea jana usiku walifanya yao baada ya kuwatuza wachezaji walifanya vema msimu huu.

Kiungo wa Chelsea Willian akiwa na moja kati ya tuzo mbili alizotwaa jana usiku.

Matajiri wa London timu ya soka ya Chelsea jana usiku ilifanya hafla fupi yakuwatuza wachezaji wake waliofanya vema katika michuano mbalimbali kwa msimu huu wa 2015/2016.

Katika tuzo hizo nyota wa Brazil, Willian amefanikiwa kufunika usiku huo baada ya kutwaa tuzo mbili kubwa moja ya kuwa mchezaji bora wa mwaka wa labu hiyo na nyingine ya kuwa mchezaji Bora Chaguo la Wachezaji wa Mwaka wa klabu hiyo baada ya kushinda usiku wa jana katika hafla iliyofanyika katika uwanja wa Stamford Bridge, London.

Mbali na Willian kushinda tuzo hizo, Eden Hazard ameshinda tuzo ya kufunga Goli Bora la Mwaka, huku kinda mwenye uwezo mkubwa Ruben Loftus-Cheek naye akishinda tuzo ya Mchezaji Bora chipukizi wa Mwaka.

Kinda mwingine mwenye ufundi mwingi kiwanjani Fikayo Tomori ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Akademi na mwanadada Katie Chapman yeye akitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Kike wa Mwaka.

Wakati huo huo Chelsea imempa ofa ya Mkataba mpya wa mwaka mmoja, Nahodha wake, John Terry na sasa ni juu yake kubaki au kuondoka Stamford Bridge msimu ujao.

Terry na wakala wake, Paul Nicholls, wamekutana na Mkurugenzi wa Chelsea, Marina Granovskaia na Mwenyekiti, Bruce Buck kwa mazungumzo katika viwanja vyao vya mazoezi vya Cobham wiki hii.

Klabu hiyo imethibitisha leo kwamba Terry anaweza kubakia baada ya Juni 30, wakati Mkataba wake utakapomalizika, ingawa Chelsea imemuachia mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 35 kuamua kama atabakia ndani ya kikosi hicho kinachotumia dimba la Stanford Bridge jijini London au ataamua kusaka maisha mahali pengine au hata kutundika daluga zake.

Msemaji wa klabu amesema; "Marina Granovskaia na Bruce Buck wamekutana na John na wakala wake na kumpa ya Mkataba wa mwaka mmoja abaki,".

"Na wakati msimu unaelekea ukingoni, haya ni maamuzi mazito kwa John na familia yake na kitu ambacho wanakifikiria kwa sasa,".

Mashabiki wa Chelsea walikuwa wakimpigia debe Nahodha huyo usiku wa Jumatano Uwanja wa Anfield wakitaka Terry aongezewe Mkataba mpya huku wakiwa wamebeba mabango yanayoonyesha mataji mengi ambayo klabu ilishinda chini ya uongozi wake.

Pamoja na kwamba umri umeenda na kiwango kimeshuka, lakini Terry bado ni kipenzi cha mashabiki wa Stamford Bridge haswa wanapokumbuka mchango wake enzi zake akicheza kwa jihadi na kuwa kizingiti kwa washambuliaji hatari langoni.