Baadhi ya mabondia wa Tanzania katika picha wakipambana katika michuano ya madola
Shirikisho la ngumi za ridhaa Tanzania BFT limesema litaandaa michuano ya taifa mabayo itakuwa na wachezaji mchanganyiko huku nafasi kubwa wakipewa mabondia vijana na chipukizi ili kuwaandaa kwa ajili ya michuano ijayo ya kimataifa
Katibu mkuu wa BFT Makole Mashaga amesema uamuzi huo umetokana na matokeo mabovu waliyopata mabondia waliyoiwakilisha nchi katika michuano ya jumuiya ya madola inayoendelea nchini Scotland
Kwa upande mwingine shirikisho la ngumi za ridhaa nchini BFT limesema linafanya uchunguzi ili kubaini sababu iliyopelekea Bondia Nasser Mafuru kutopanda ulingoni katika michuano ya Jumuiya ya Madola hali iliyolifedhehesha shirikisho hilo.
Katibu mkuu wa BFT Makole Mashaga amesema wanasubiri ripoti ya tukio hilo kutoka kwa viongozi walioambatana na mabondia hao Scotland japo wamekuwa wakipokea taarifa tofauti kutoka vyanzo mbalimbali na hawatafumbia macho tukio hilo na atakayehusika awajibishwe
Naye mmoja wa mabondia waliowahi kushiriki michuano ya jumuiya ya madola iliyofanyika nchini New Zealand mwaka 1992 Anthony Mwang’onda amesema lawama zote kuhusiana na matokeo ya mabondia walioshiriki mashindano hayo mwaka huu anazitupa kwa kamati ya olimpiki Tanzania TOC.
Mwang’onda amesema hayo kutokana na kile anachodai TOC hawakuzingatia ushauri wa makocha na mabondia wakongwe katika maandalizi ya kiufundi na uteuzi wa mabondia hao jambo ambalo lilizua mvutano na wao kuiachia TOC iamue na matokeo ndiyo haya hakuna medali.