BBall kitaa chini ya mataa.
Mashindano ya mpira wa kikapu ya BBall Kitaa ambayo hufanyika kila Ijumaa ya kwanza ya mwezi, maarufu kama BBall Kitaa chini ya mataa (Friday Night Games), yatafanyika Ijumaa ya juma hili kwa kushirikisha timu za US Marine kutoka Marekani, Mbeya Flames kutoka Mbeya na mabingwa wa BBall kitaa mwaka huu East Zone 4 ya Temeke.
Akiongea leo jijini Dar es salam, mratibu wa mashindano hayo Kalabani Kalabani ameelezea jinsi walivyojipanga kuhakikisha usalama utakuwepo hasa ukizingatia michuano hiyo itafanyika usiku.
Bwana Kalabani amesema usalama utakuwa wa kutosha kwani kutakuwa na polisi pamoja na askari kanzu. Pia kutakuwa na usafiri maalum wa mabasi kutoka uwanjani hapo mpaka Kariakoo ili kupunguza usumbufu kwa mashabiki.
Naye nahodha wa timu ya East Zone 4 ambao ndio mabingwa wa BBall kitaa kwa miaka miwili mfululizo, Murshid Mudricat , amesema timu yake iko tayari kuzikabili timu zote itakazokutana nazo na wao wanataka kuwaonesha watu kwamba ubingwa wao sio wa kubahatisha.