
Kocha wa Azam FC Hans Van Der Pluijm
Hans amebainisha hilo leo baada ya mazoezi ya asubuhi ambapo, ametoa sifa kwa wachezaji wake kuwa wanajitoa kila mmoja kuhakikisha timu inafanya vizuri kwenye mashindano inayoshiriki ikiwemo ligi kuu.
“Natoa sifa kwa wachezaji namna wanavyofanya mazoezi, namna wanavyofanya kazi inaonesha wameelewa ninachowaekeza na wako tayari kila mmoja na wanacheza kitimu, hili ndio la muhimu kwenye mpira,” amesema Van Der Pluijm.
Uhalisia wa maneno ya Hans unaonekana wazi kwenye matokeo ya Azam FC kwenye ligi kuu soka Tanzania bara ambapo hadi sasa haijapoteza mchezo na ipo kileleni ikiwa na alama 27 kwenye mechi 11.
Azam FC ilikuwa icheze mchezo wake wa 12 wa ligi kuu wikiendi hii ugenini dhidi ya Singida United, lakini mechi hiyo imesogezwa mbele ili kupisha maandalizi ya timu ya taifa Taifa Stars inayojiandaa kucheza na Lesotho kuwania kufuzu AFCON 2019.