Monday , 11th Jul , 2016

Uongozi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, umetangaza rasmi kuwatema wachezaji sita kwa awamu ya kwanza huku nyota wawili wakifeli majaribio.

Aliyekuwa Mlinda mlango wa Azam FC, Ivo Mapunda

Nyota hao walioachwa ni makipa Ivo Mapunda, Khalid Mahadhi aliyekuwa ametolewa kwa mkopo Mafunzo ya Zanzibar, mabeki Said Mourad, Racine Diouf kutoka Senegal pamoja na washambuliaji mrundi Didier Kavumbagu na Allan Wanga kutoka nchini Kenya.

Afisa Habari wa Azam FC Jaffar Idd amesema wachezaji hao wameachwa wakiwa wamepata stahiki zao kwa wale ambao waliokuwa na mikataba.

Alisema mbali na wachezaji hao, pia wachezaji wawili kati ya wanne waliokuwa kwenye majaribio nao wameachwa rasmi ambao ni beki wa kushoto kutoka Ghana, Nurudeen Yusif aliyetokea Medeama ya huko na kiungo mshambuliaji David Wirikom (Cameroon).

Jaffar amesema, wawili hao wamepewa majibu ya kufeli majaribio yao kufuatia Kocha Mkuu Zeben Hernandez kutoridhishwa na uwezo wao kwa siku nne walizofanya mazoezi na kikosi cha Azam FC.

Jaffar amesema, wanatarajia kuwapokea wachezaji wengine wa kimataifa ndani ya siku mbili au tatu zijazo kwa ajili ya majaribio yote ni katika kuendelea.

Wachezaji wanaoendelea kwenye majaribio ni makipa Daniel Yeboah (Ivory Coast) na Juan Jesus Gonzalez (Hispania), ambao wanawania nafasi moja ya usajili katika eneo la golikipa.