Monday , 8th Feb , 2016

Mechi mbili za viporo za Azam FC dhidi ya Prisons na ya Azam FC dhidi ya Mwadui FC zimepangiwa tarehe mpya.

Azam FC itamenyana na Prisons Februari 24, mwaka huu uwanja wa Sokoine mjini Mbeya kabla ya kumenyana na Stand United Machi 16, uwanja wa Chamazi Complex jijini Dar es salaam.

Timu zote zitaendelea na ratiba iliyopo ya Ligi Kuu, Azam FC ikimenyana na wenyeji Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Jumapili, wakati Stand United wataikaribisha Simba SC Jumamosi mjini Shinyanga na Prisons wataifuata Mwadui FC Jumapili.

Azam FC iliondolewa kwenye ratiba ya Ligi Kuu wiki mbili zilizopita ili iende kucheza michuano maalum ya kirafiki nchini Zambia kwa ajili ya kujiandaa na Kombe la shirikisho barani Afrika.

Katika michuano hiyo iliyoshirikisha pia timu za wenyeji, Zanaco FC na Zesco United pamoja na Chicken Inn ya Zimbabwe, Azam FC iliibuka bingwa.

Baada ya kurejea nchini, Azam FC ilicheza mechi yake ya kwanza jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi na kushinda 1-0 dhidi ya Mwadui FC, bao pekee la Kipre Herman Tchetche dakika ya 18.