Mcheza Tennis raia wa Uingereza Johanna Konta amefanikiwa kuwa miongoni mwa wachezaji 30 bora wa mchezo huo kwa upande wa wanawake kutokana na hatua aliyofikia katika michuano ya wazi ya Australia iliyomalizika jana.
Konta amepanda nafasi 19, kutoka nafasi ya 47 hadi nafasi ya 28 baada ya kufikia hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.
Wakati Konta akipanda, muingereza mwingine Heather Watson ambaye anashikilia nafasi ya pili nchini humo, ameporomoka nafasi 6 kutoka 79 hadi 85 kutokana na kutolewa katika mashindano hayo raundi ya kwanza.
Katika orodha hiyo mpya, bingwa mpya wa michuano ya wazi wa Australia Angelique Kerber amepanda hadi nafasi ya pili akiwa nyuma ya Serena Williams ambaye ameendelea kung’ang’ania nafasi yake ya kwanza.
Kerber raia wa Ujerumani alifanikiwa kumshangaza mchezaji namba moja, Serena Wiliams na kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza, huku akikatisha ndoto za Serena za kufikia rekodi ya kutwaa mataji 22.
Kwa upande wa wanaume, Novak Djokovic baada ya kutwaa taji la Australia, ameendelea kubaki katika nafasi ya kwanza akifuatiwa na Andy Murray katika nafasi ya pili.
Nafasi ya tatu iko kwa Roger Federer, nafasi ya nne ni Stan Wawrinka nafasi ya tano inashikwa na Rafael Nadal huku muhispania mwingine David Ferrer akiwa nafasi ya sita.





