Timu ya Ashanti United
Michuano ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2013/14 imefikia tamati leo (Aprili 19, 2014) kwa timu zote 14 kuwa viwanjani, na kushuhudia Ashanti United ikiteremka daraja kurudi ligi ya daraja la kwanza msimu ujao.
Ashanti United iliyopanda daraja katika msimu huu unaomalizika, imefungwa na Prisons ya Mbeya bao 1-0 katika mchezo wa funga dimba uliopigwa leo katika uwanja wa Jamhuri morogoro.
Katika Mechi hiyo Ashanti ilikuwa ikitakiwa kupata ushindi wa aina yoyote ili kuiacha Prisons ambayo ilikuwa ikilingana nayo point (25).
Kwa matokeo hayo Prisons imefikisha point 28 na kuiacha Ashanti ikiunga na timu za Rhino Rangers na Oljoro JKT.
Mabingwa wapya Azam waliokabidhiwa kombe lao leo katika uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam wamenogesha sherehe zao kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Ruvu, na hivyo kumaliza ligi wakiwa na point 62, wakiwa hawajapoteza mchezo hata mmoja.
Katika mchezo uliowakutanisha watani wa jadi Yanga na Simba uwanja wa Taifa DSM, matokeo ni kwamba timu hizo zimetoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1 katika mchezo uliokuwa na vioja vya hapa na pale.
Simba ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Haruna Chanongo dakika ya 76 kabla ya Simon Msuva kuisawazishia Yanga katika dakika ya 86.
Katika hali ya kushangaza, Baadhi ya wachezaji wa Yanga wakiongozwa na Didier kavumbagu, walivamia na kuliondoa golini taulo la Golikipa wa Simba Ivo Mapunda kwa madai kuwa linachangia kukosekana kwa magoli.
Baada ya kavumbagu kuliondoa taulo hilo, palizuka tafrani ndogo iliyosababisha mpira kusimama kwa dakika kadhaa kabla ya Ivo Mapunda kupewa taulo lingine na mchezo kuendelea huku Didier kavumbagu akizawadiwa kadi ya njano.
Pasipo kufahamu alitokea wapi, shabiki mmoja wa Yanga alishuka dimbani na kuliondoa taulo lile na kukimbia nalo jukwaani kabla ya kudhibitiwa na askari.
Kwa matokeo hayo Yanga imemaliza ligi ikiwa nafasi ya pili na point 56 wakati Simba wakiwa nafasi ya 4 na point 38, sawa na Kagera Sugar, lakini ikiizidi tofauti ya magoli.
Matokeo ya mechi nyingine zilizopigwa leo ni kwamba Rhino Rangers imefungwa mabao 2-0 na Ruvu Shooting (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora), Mbeya City imeifunga Mgambo Shooting bao 1-0 katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Oljoro JKT na Mtibwa Sugar zimetoka sare ya bao 1-1 katika Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha na Coastal Union imechezea kipigo cha bao 1-0 toka kwa Kagera Sugar katika uwanja Mkwakwani, Tanga.