Thursday , 1st Nov , 2018

Mshambuliaji wa klabu ya Mbeya City, Eliud Ambokile amefunguka juu ya tetesi za kusajiliwa na klabu za Simba na Yanga katika dirisha dogo la usajili la ligi kuu Tanzania bara (TPL) linaloendelea.

Mshambuliaji wa Mbeya City, Eliud Ambokile

Eliud Ambokile ndiye mchezaji anayeongoza kwa sasa katika listi ya wafungaji bora wa ligi, akiwa na mabao 8 akifuatiwa na Emmanuel Okwi ambaye aliibuka mfungaji bora msimu uliopita.

Akizungumza na www.eatv.tv, Ambokile amesema kuwa kwa sasa yupo chini ya mkataba na klabu yake ya Mbeya City na kusisitiza kuwa endapo vigogo Simba, Yanga na Azam Fc wanamuhitaji, wamalizane na uongozi wa klabu yake.

"Kama wananihitaji kikubwa wawafuate viongozi wangu kwa maana mimi bado niko kwenye mkataba na Mbeya City. Wakimalizana na viongozi mimi sina tatizo tutamalizana tuu", amesema Ambokile.

Aidha mshambuliaji huyo amezungumzia kuhusu rekodi ya mshambuliaji, John Bocco kufikisha mabao 100 ya ligi kuu, rekodi aliyoifikia msimu huu na kusema kuwa anampongeza kwakuwa sio kazi rahisi kuifikia idadi hiyo ya mabao, akisema kuwa nayeye atafikia katika hatua hiyo.

"Uwezo wa kufikia idadi ya mabao 100 ya Bocco ninao kwasababu nina nia na kuhusu rekodi yake kwenye ligi kwangu mimi ninampongeza sana kwasababu haikuwa rahisi kwake", ameongeza.