Mlinda Mlango wa Azam FC, Aishi Salum Manula
Azam FC jana iliacha point tatu Mkwakwani jijini Tanga baada ya Mpira wa adhabu uliopigwa na beki wa kulia Miraj Adam katika dakika ya 67 baada ya Mlinda Mlango Aishi kuudaka mpira na kulala nao kwa muda mrefu huku akiugulia maumivu badala ya kuutoa nje kwanza na mwamuzi Vincent Mlabu kutoka Morogoro aliyesaidiwa na Gasper Ketto na Mohammed Mkono akawaadhibu Azam.
Aishi amesema, inasikitisha sana kuona soka la Tanzania lina shindwa kuendelea mbele pia inasikitisha kuona nchi jiran zikisonga mbele kisoka kama Uganda na Rwanda wakati Tanzania imepata uhuru mapema na inabaki kuona nchi jirani zikisonga mbele huku ikibaki palepale kama sio kurudi nyuma.
Aishi amesema, alikuwa anajiuliza ni kwanini Tanzania ina wachezaji wazuri na kila wanapoenda wanasifiwa kwamba ni timu nzuri lakini anashindwa kuelewa ni kwanini wanashindwa kufanya vizuri.
Aishi amesema, binafsi anaangukia upande wa waamuzi kwani waamuzi wa Tanzania ni tofauti na waamuzi wengine duniani kote na anashindwa kufahamu ni sheria gani ambazo waamuzi wa Tanzania wanazitumia kuendeshea ligi kwani makosa wanayoyafanya viwanjani si ya kawaida na si mara chache na kwamba imekuwa ni kama desturi yao.
Aishi amehoji, endapo Shirikisho la Soka nchini TFF linaangalia kama ni kweli waamuzi huwa wanakidhi vigezo na masharti mpaka wanapewa vyeti kwa ajili ya kusimamia sheria 17 za mpira wa miguu.
"Je, kabla ya kuanza ligi huwa TFF wanawapeleka hospital kwa ajili ya kucheki afya zao?. Mfano: KUPIMA MACHO KAMA YANA UWEZO WA KUONA MBALI"
Aishi amesema, katika suala la mpira wa kuotea, ndo kuna makosa makubwa na kwamba hilo ni janga kati ya majanga walionayo waamuzi wa Tanzania.
Aishi amesema, inawezekana waamuzi wakawa wanalaumiwa kuwa ni wabovu lakini kumbe hawaoni mbali.
Amemtaka Rais wa TFF Jamal Malinzi kuangalia jipu hilo kubwa na ambalo limeiva na linalosubiri kutumbuliwakwani waamuzi ni kitu kikubwa katika kuinua soka la nchi.
Akizungumzia tukio la mchezo wa jana, Aishi amesema kuwa alipodaka mpira alipatwa na maumivu makali baada ya kujigonga chini na kumsababisha kushindwa kuinuka na kutupa mpira nje, badala yake akanyoosha mkono na kumuonesha mwamuzi kuwa amepatwa na tatizo.
Anasema jambo la kushangaza ni mwamuzi huyo kupuliza filimbi na kuonesha faulo kuelekea lango la Azam FC.
Aishi amesema, tukio kama hilo limewahi kutokea uwanja wa Karume ambapo baada ya kipa kupata tatizo akiwa na mpira alionesha ishara kuwa kapatwa na maumivu na mwamuzi alipuliza filimbi na kuwaita madktari,
Anasema baada ya kumaliza kutibiwa kipa alichukua mpira na kuuachia chini akiashiria katoa fair play.







