Wednesday , 2nd Dec , 2015

Msanii Matonya ambaye kwa sasa amerudi kwenye game baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu, amewataka wasanii wachanga kutia bidii na kujituma katika kazi zao, ili waweze kufanikiwa.

Matonya ameyasema hayo alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa Radio na kusema kwamba wasanii wenyewe ni lazima wajiongeze na sio kusubiria kusaidiwa na watu wenye uwezo kwenye fani.

“Kwanza kabisa ni kujiongeza binafsi, uwe unatamani kufanya kitu kufika pale kabla mtu hajakusaidia inabidi mwenyewe ujisaidie, halafu ukishajisaidia labda kutatokea support kutokana na ule muonekano na nguvu ambayo umetoa mpaka pale umefika, juhudi binafsi inatoka kwa mtu binafsi, hakuna mtu atatoka aseme bwana nakushika mkono anakunawisha na kukulisha chakula, hapana, atakupa line moja ya pili unatakiwa ujiongeze”, alisema Matonya.

Matonya ameendelea kusema kwamba anatamani kuona vipaji vinaongezeka ili kukuza muziki na sehemu ambazo wasanii hao wanatokea, hivyo wao kama wasanii wakongwe watalifanyia kazi na kuangalia ni jinsi gani wanatekeleza hilo.

“Sijui ni nini lakini tunatamani sana vipaji viongezeke ili kukuza ule muziki na mji na sehemu nyingine ambayo watu wanatokea, kwa hiyo kifanyiwe kazi, tutafanyia kazi pia kama sisi wahusika, tuone namna gani tunaweza kupush ile town tuone inakaa vizuri”, alisema Matonya.