Katika taarifa yake iliyotolewa jioni ya leo na kusainiwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa wizara Zawadi Msalla, amesema kuwa wizara hiyo kwa dhamana yake katika tasnia ya sanaa, imefuatilia kwa karibu suala hilo kwa kuwa lina muelekeo wa jinai na kwamba hashikiliwi katika kituo chochote cha polisi.
"Hata hivyo taarifa kutoka vyombo vya dola zinathibitisha kuwa Roma Mkatoliki hashikiliwi katika kituo chochote cha polisi".Amesema Zawadi.
Amesema kutokana na hali hiyo, wizara imewaomba wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa zozote zitakazo saidia kujua alipo msanii huyo.
Hata hivyo, mapema leo, baadhi ya wasanii wa muziki na filamu nchini wamezungumza na wanahabari kuhusiana na hilo, na kutoa taarifa kuwa wamezunguka katika vituo karibu vyote vya polisi jijini dar es Salaam lakini hawajaweza kupata taarifa zozote kumuhusu Roma, huku wakidai kuwa Kamanda wa Polisi Simon Sirro ameahidi kulitolea ufafanuzi siku ya kesho Jumamosi.