Wednesday , 19th Jul , 2017

Msanii kutoka kundi la Navy Kenzo, Aika ameweka wazi siri ya kudumu kwenye mahusiano na mpenzi wake wa muda mrefu (Nahreel) ambaye pia ni mwanamuziki  na kusema kuwa kwao wakweli na wawazi ndiyo siri ya mafanikio yao.

Akizungumza na 5Selekt ya EATV kwa njia ya Skype Aika amesema kwamba wamekuwa makini sana katika kuzuia maneno kuhusu mahusiano yao yasizungumzwe nje.

"Sisi tupo real sana. Siku skendo kuhusu sisi ikitokea ikavuma ndivyo itakuwa hivyo hivyo itakavyosikika lakini kwa kuwa sisi ni watu wazima tunajua jinsi ya kuzungumza na kutulizana yakitokea matatizo kati yetu na pia huwa tunatambua jinsi gani ya kufanya maneno yetu ya ndani yasitoke nje, hii ndo siri tuliyoishi nayo kwa miaka yote tuliyokuwa kwenye mahusiano," alisema Aika.

 

Kwa upande wa Nahreel ambaye ni mpenzi wa Aika, mwanamuziki na mtayarishaji amesema kwamba watu watarajie familia yake kuongezeka muda wowote kwani mipango imekwisha anza.

"Familia yangu na Aika mtarajie kuongezeka muda wowote kwa sababu sisi wawili hatutaweza kuishi kwenje mjengo mkubwa aina hii peke yetu" Nahreel.

Kwa upande wa mauzo ya albamu waliyoitoa mwaka jana Nahreel amesema kwamba "Albamu imetuletea mafanikio mengi sana kwenye muziki wetu, pesa, lakini imetusaidia kututangaza sehemu nyingi sana na bila hata ile albamu tusingeweza kufika hata Israel na sehemu nyingine duniani" alisema.