Friday , 13th Nov , 2015

Msanii ambaye ni rapa Nikki Mbishi amesema wanaopinga alichokiandika kwenye ukurasa wake wa Instagram hawaelewi yaliyomo kwenye tasnia ya muziki wa Bongo.

Nikki Mbishi ameyasema hayo baada ya timu ya Planet Bongo ya East Afica Radio kufanya mazungumzo naye kufuatia ujumbe aliouandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

“Ile ni experience, ambayo kwa upeo mdogo kwa mtu ambaye hayupo kwenye industry anaweza akasema hivyo, watu wanatakiwa wajue nilichokisema ni kweli kwamba muziki huu wanaaua, na wanachokifanya wao ni muziki unakuwa na manufaa ya wachache:, alisema Nikki Mbishi.

Nikki Mbishi aliendelea kusema kwamba wasanii walioingia bungeni wamejisahau kuhusu matatizo yanayoikabili sanaa, ambayo walikuwa wanayapigia kelele kabla ya kuwa wabunge.

“Wito mwingine natoa, naona sasa hivi waheshimiwa ambao walikuwa wasanii wameongezeka bungeni, hili nalitoa kwao, walivyokuwa wasanii wao walijifanya wanajua sana kujifanya wanapigia kelele haya mambo, leo hii wamesahau nao, hilo nawaambia ukweli wao wameshajisahau, vitu vingi watu wanatakiwa wavijue, watu wasiwapeleke peleke tu kwa sababu wameshapata walichokuwa wanakitaka”, alisema Nikki Mbishi.

Leo asubuhi Nikki Mbishi aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram akilalamikia mfumo uliopo kwenye muziki na kudai kuwa ni wa urasimu na kujuana.