Monday , 17th Dec , 2018

Muandaaji wa filamu nchini, Timoth Conrad 'Tico' amempa makavu muigizaji maarufu wa Tanzania, Rammy Galis aliyeachia filamu yake wikiendi hii kuwa ubovu wa filamu yake utawakosesha pesa watu wengine wanaotegemea tasnia hiyo kuendesha maisha yao akiwemo yeye.

Rammy Galis akiwa na Agness Masogange enzi za uhai wake.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Timoth amebainisha kuwa Rammy Galis pamoja na 'team' yake wanafahamu kuwa filamu yao ni mbovu lakini pia haikustahili kuoneshwa katika jumba la kuoneshea filamu.

Akitoa kasoro za filamu hiyo ya 'Hukumu' ambayo ndani yake ameigiza marehemu Agness Masogange, Timoth ameendelea kusema kwamba filamu hiyo imefanywa kiholela sana na yeye mwenyewe Galis na team yake wanajua kuwa sauti imefanyiwa studio lakini imefanywa hovyo kiasi cha kujirudia rudia bila mpangilio.

"'Mixing' ilikua mbovu, picha, stori yakuunga unga Dah! Sipendi niongelee 'details' zote lakini kwa ufupi filamu ya 'Hukumu' ni miongoni mwa filamu mbaya ambazo hazikustahili kuoneshwa kwenye 'cinema'," amesema Timoth.

Muongozaji wa filamu Timoth Conrad

Pamoja na hayo Timoth ameongeza kuwa, "Sio freshi jamani bwana Rammy kumbuka tunaoumia ni sisi endapo watazamaji wakikosa imani na sisi wote tutapata wapi hela wakati tunajua, mfumo wa DVD siku hizi majanga, 'online streaming' bado, wanachoweza nikuja kwenye cinema, sasa tunavyozingua inakuaje? Unadhani watakuja tena wakisikia Bongo movie inazunduliwa? Hata tukijinadi oooh uzinduzi wa kitaifa, hawaji ng'o. Tusichukulie poa jamani huu ndo ugali wetu. Siongei kwa ubaya lakini naongea kwa uchungu! Nilipokosea naomba mnisamehe".

Aidha baada ya kuzungumza na www.eatv.tv kuhusu njia aliyotumia kumfikishia ujumbe Rammy, Timoth amesema kwamba amelazimika kutumia njia hiyo kwa kuwa mara nyingi huwa wanaambizana pasipo watu kujua na imefika wakati jamii inapaswa kufahamu kuwa wapo watu wanaopambania sanaa na kwamba kwa sasa mabadiliko hayawezi kufanyika kimya kimya.

"Mimi na Rammy ni marafiki wa miaka mingi na maoni yangu hayawezi kusababisha bifu kati yetu. Kwa mtu anayeweza kuchukulia maoni yangu kwa upande chanya yatamjenga na mabadiliko yatatokea. Mimi kutoa maoni kama yale ni kitu cha kawaida hasa katika kipindi hiki tunachotaka kuleta mabadiliko".

Mbali na hayo, Timoth amesema kwamba Wasanii wengi wanakwama hasa katika kuchukua hatua za mabadiko na kwamba wengi wao wanaharaka za kutoa filamu pasipo kuangalia kwa sasa ni kitu gani kinatakiwa na watazamaji.

Kabla ya uzinduzi huo Rammy aliweka wazi kwamba sehemu ya mapato ya filamu hiyo atayapeleka kumsaidia mtoto wa Agness Masogange ambaye alifariki April 20 mwaka huu. Hata hivyo www.eatv.tv ilipomtafuta Rammy Galis kuzungumzia maoni hayo kutoka kwa Muongozaji wa filamu Timoth simu yake haikupatikana.

Timoth ambaye ni Muongozaji wa filamu kutoka 'Timamu Production' Disemba 1 aliachia filamu yake iliyokwenda kwa jina la 'Sema' iliyowakutanisha waigizaji wa vichekesho , Ebitoke, Bwana Mjeshi pamoja na Mr. Beneficial.