Friday , 31st Jul , 2015

Msanii wa muziki Zuena Mohamed maarufu zaidi kama Shilole amefungiwa kujihusisha na sanaa katika kipindi cha mwaka mmoja ili kujirekebisha kimaadili kwa kutumbuiza jukwaani akiwa amevaa nusu utupu katika onyesho lake huko Ubelgiji mwezi mei mwaka huu

Shilole

Akiitolea ufafanuzi hatua hii, katibu wa BASATA Godfrey Mngereza amesema, Baraza limeamua kuchukua hatua hiyo kufuatia ahadi ya Serikali katika Bunge la Bajeti tarehe 28 Mei, ambapo Mhe. Juma Nkamia alieleza kuwa taratibu zote zitachukuliwa dhidi ya msanii huyu, BASATA wakiwa ndio watekelezaji na wasimamizi wa masuala ya kisanaa, wakizingatia maelekezo ya sheria mama inayozuia ukiukaji wa maadili.

Mngereza pia amegusia taarifa za awali za msanii huyo kuitwa na BASATA, kuonywa na kumaliza suala hilo ambapo amesema hatua hiyo haikuwa rasmi, ikiwa si mara ya kwanza kwa BARAZA hilo kumuita Shilole na kumuonya kutokana na vitendo vya uvunjaji wa maadili jukwaani.

Kufuatia kifungo hiki, Shilole hatatakiwa kujihusisha na sanaa ya aina yoyote ile, iwe ni muziki ama uigizaji ambao pia ni fani yake nyingine, BASATA ikiweka bayana kuwa imeamua kuchukua hatua hii dhidi ya Shilole ikiwa ni kipindi kimepita baada ya tukio lenyewe kutokana na kuzingatia kufuatilia taratibu zote stahiki mpaka kufikia uamuzi huo.

eNewz tunaendelea kumtafuta Shilole kusikia upande wake wa maelezo juu ya hatua hii dhidi yake.