Zitto Kabwe
Katika kuikumbuka siku hii muhimu, Kiongozi wa Chama cha ACT-wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ametumia kupaza sauti juu ya hali ya demokrasia ya vyama vya siasa ilivyo nchini hasa katika Muswada wa Mabadiliko ya Sheria za Vyama Vya Siasa uliopendekezwa.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Zitto Kabwe ameandika, "1961 tulipata Uhuru na kujitawala. 1965 tukawa nchi ya Chama kimoja cha Siasa. 1992 tukagundua makosa na kurejea kwenye siasa ya vyama vingi vya siasa. 2018 umependekezwa muswada wa vyama vya siasa ili ifikapo 2019 turudi kwenye ‘defacto’ Chama Kimoja Cha Siasa".
Pia katika kupinga muswada huo, Zitto amesema kuwa chama chake cha ACT pamoja na vyama vingine 14 vimeazimia kufanya mkutano wa pamoja na wanahabari leo jijini Dar es salaam ili kutoa tamko la pamoja kuhusu Mswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa.
Ikumbukwe kuwa, (Jumanne, Novemba 20, 2018) Rais Dkt. John Magufuli aliagiza kiasi cha shilingi milioni 995.182 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha sherehe za Uhuru mwaka huu zitumike kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mkoani Dodoma.
Taarifa hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu wakati alipokutana na viongozi waandamizi wa mkoa wa Lindi pamoja na wilaya zake katika kikao cha maandalizi ya shughuli za kuzima Mwenge kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Alisema hospitali hiyo itakayojengwa katika eneo la kati ya barabara ya kwenda Hombolo na Chamwino kwenye barabara ya kwenda Dar es Salaam itakuwa inawahudumia wakazi wa mkoa wa Dodoma pamoja na wananchi wengine watakaokuwa mkoani humo.
Kadhalika, Waziri Mkuu alisema kuwa Rais Dkt. Magufuli amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya waandae matukio watakayoyatekeleza katika maeneo yao yatakayoashiria maadhimisho ya siku ya Uhuru ikiwemo kufanya usafi maeneo ya wazi au kwenye hospitali.