
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi, Mawasiliano ya Umma na Uenezi wa chama hicho, Ado Shaibu imesema kuwa kiongozi huyo amekamatwa na Polisi wa kituo cha Osterbay jijini Dar es salaam.
"Kiongozi wa Chama, ndugu Zitto Kabwe amekamatwa na Polisi wa Kituo cha Polisi Oysterbay muda huu kwa maelezo kuwa anakwenda kuhojiwa juu ya mauaji ya Polisi na raia yaliyotokea kwenye Kijiji cha Mpeta, wilayani Uvinza, mkoani Kigoma, mauaji ambayo Zitto alitaka Jeshi la Polisi liyatolee maelezo katika mkutano wake na Wanahabari juzi Jumapili, Oktoba 29, 2018", amesema Shaibu.
Hayo yanajiri wakati jana Jumanne, Oktoba 30, 2018, Kamanda wa polisi mkoani Kigoma, Martin Ottieno katika mkutano wake na waandishi wa habari alisema kuwa tuhuma alizotoa Zitto hazina ukweli wowote dhidi ya mauaji hayo hakuna watu 100 waliouawa na kusisitiza kuwa ni upotoshaji unaofanywa na wanasiasa.
“Hakuna watu mia moja waliouawa. Tunamtaka Zitto aonyeshe vielelezo vya hayo anayosema au aje atuonyeshe makaburi ya watu hao anaosema wameuawa Kigoma”, alisema Kamanda Ottieno.