Friday , 26th Feb , 2016

Zao la korosho limetajwa kushuka kibiashara kwa asilimia 22.8 katika msimu huu uliomalizika wa 2015/2016 ukilinganisha na misimu mingine iliyopita, hali ambayo imesababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na ucheleweshwaji wa pembejeo.

Korosho

Hayo yameelezwa na meneja wa uchumi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (B.O.T) tawi la Mtwara, Mussa Mziya, wakati akiwasilisha taarifa ya uchumi wa mkoa wa Mtwara katika kikao cha Baraza la Ushauri la Mkoa (RCC), na kudai kuwa msimu wa 2013/2014 kulikuwa na ongezeko la asilimia 53.8.

Mziya amesema kuwa kwa kipindi cha miaka miwili zao hilo la korosho lilipanda kwa asilimia 53 lakini kutokana na kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo katika wilaya ya Tandahimba limesababisha kuyumba kidogo kwa zao hilo mwaka huu.

Aidha, amesema kuwa pamoja na changamoto hiyo, mfumo wa stakabadhi ghalani unaotumika katika ununuzi wa zao hilo umekuwa ukifanya vizuri kiasi cha kuzidi kuaminiwa na wakulima ambapo kwa mujibu wa utafiti walioufanya unaonesha kuwa asilimia 87 ya wakulima wanaukubali.