Tuesday , 9th Feb , 2016

Jeshi la Polisi nchini Tanzania limesema kumekuwa na udhibiti hafifu wa silaha katika mipaka ya nchi hali inayochangia kwa kiasi kikubwa kuzagaa kwa silaha kutokana na kuwa na mipaka mingi nchini.

Akizungumza na watendaji wa wizara ya mambo ya ndani ya nchi, idara na taasisi za serikali na zisizo za serikali pamoja na wadau mbalimbali, mratibu wa kitaifa wa kudhibiti silaha nchini kuhusu sheria mpya ya umiliki wa silaha iliyopitishwa Novemba mwaka jana Kamishna Msaidizi wa Polisi Charles Lulaya amesema uwepo wa mipaka mingi ni changamoto kubwa katika kudhibiti kuzagaa kwa silaha.

Kamishna Msaidizi Lulaya amesema jeshi la polisi limekuwa likifanya juhudi mbalimbali za kukabiliana na kuzagaa kwa silaha nchini ikiwa ni pamoja na kuziteketeza silaha haramu mara wanapozikamata katika mipaka ya nchi.