Wednesday , 16th Mar , 2016

Makamu wa Rais wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan ameziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha vituo vyote vya afya vyenye huduma za uzazi vinaweka huduma za dharura kwa wajawazito haraka iwezekanavyo mara baada ya bajeti ya mwaka 2016.

Mh. Samia amesema hayo leo jijini Dar es salaam wakati wa ufunguzi wa siku ya utepe mweupe nchini yenye lengo la kuwakumbuka wakina mama wajawazito na waliopoteza maisha siku ya kujifungua.

Mh. Samia ameonyesha kusikitishwa kwake juu ya ongezeko kubwa la vifo vya wajawazito na watoto wadogo ambapo pia amebainisha kwamba serikali haitafumbia macho suala hilo na kuliacha liendelee.

Kwa upande wake mwakilishi wa waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto Mh. Ummy Mwalimu, Profesa Mohamedi Bakari amesema kuwa kila siku wajawazito 24 wanaojifungia hufariki na wengine kupata vilema vya maisha na kuwa tayari wizara yake imeshaandaa mikakati mbali mbali ya kupunguza na kutokomeza kabisa tatizo hilo.