Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa anatarajiwa kuondoka nchini leo jioni kwenda London.
Akizungumza na waandishi wa habari leo mchana, Waziri Mkuu alisema anaenda kumwakilisha Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli kwa sababu siku hiyo hiyo, atalazimika kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Museveni.
Mhe. Majaliwa amefafanua kwamba rais Dk. Magufuli ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na siku hiyo hiyo, mmoja wa marais wa nchi wanachama anaapishwa, kwa hiyo amelazimika kwenda kuhudhuria sherehe hizo.
Akizungumzia kuhusu mada ya mkutano huo, Waziri Mkuu amesema Tanzania inafanya vema katika mapambano dhidi ya rushwa na kwamba baadhi ya nchi zimeanza kuvutiwa na juhudi ambazo Serikali imekuwa ikichukua.
Waziri Mkuu ataambatana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kimataifa na Kikanda, Balozi Dk. Augustine Mahiga, Mkurugenzi wa TAKUKURU, Bw. Valentino Mlowola, wataalamu wa sekta ya rushwa na wanasheria.