Wednesday , 2nd Dec , 2015

Waziri Mkuu Kasim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi watatu kutoka nchi za China, Sudan Kaskazini na Korea Kusini ambao wote walimuhakikishia Waziri Mkuu kusaidiana na Serikali ya Tanzania katika kuleta maendeleo.

Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa akisalimiana na balozi wa China Nchini Dkt. Lu Youqing

Akizungumza na Waziri Mkuu balozi wa China, Dk. Lu Youqing amesema serikali itaendelea kuisaidia Tanzania kwenye sekta za uendelezaji viwanda, miundombinu, maji, afya na elimu ikiwa ni ishara kuendeleza mahusiano ambayo yamekuwepo kwa muda mrefu baina ya China na Tanzania.

Amesema Tanzania imeteuliwa kuwa miongoni mwa nchi tatu ambazo zitasaidiwa na China kuendeleza viwanda na kwamba makubaliano ya mpango huo yatafikiwa kwenye mkutano wa uwekezaji baina ya China na nchi za Afrika (FOCAC - 6) unaotarajiwa kuanza Desemba 4, mwaka huu jijini Johannesburg, Afrika Kusini. .

Naye Balozi wa Sudan Kaskazini. Dk. Yassir Mohamed Ali alisema nchi yake inao madaktari wengi na kwamba kumekuwa na majadiliano ya kuona ni jinsi gani wanaweza kuja kuongeza nguvu kwenye sekta ya afya.

Kwa upande wake Balozi wa Korea Kusini, Bw. Chung Il ambaye pia alitumia fursa hiyo kuagana na Waziri Mkuu Majaliwa, alisema anatumaini kuona ubalozi wa Tanzania ukifunguliwa nchini mwao katika muda siyo mrefu.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na mabalozi hao , ofisini kwake, Magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu aliwashukuru mabalozi hao kwa pongezi walizokuja kumpatia na kuahidi ushirikiano zaidi pamoja na nchi hizo.