Friday , 22nd Jan , 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ndiyo kitovu cha nchi hivyo ameitaka ihakikishe inaisimamia vizuri mikoa na halmashauri ili Serikali iweze kupata matokeo mazuri na tarajiwa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wakurugenzi, wakuu wa taasisi na watumishi wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwenye mkutano uliofanyika ofisi ya TAMISEMI mjini Dodoma ambapo amesema kila Mtanzania ameelekeza jicho lake pale kwa sababu anasubiri kupata huduma ya msingi.

Waziri Mkuu amesema jukumu kubwa lililopo hivi sasa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni kuhakikisha kuwa zinabuni vyanzo vipya vya mapato na kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Aidha Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kuwahudumia ipasavyo Watanzania wenye uelewa tofauti na matakwa tofauti na kwa kuanzia Serikali imeanza kuwajenga watumishi wa Serikali kutambua kuwa wao ni wahudumu wa wananchi hivyo inawapasa kuwahudumia vema.

“Lazima tujenge moyo wa huruma wa kuwahudumia wenzetu, anapokuja mwananchi msikilize, mhudumie na mwelekeze eneo sahihi ili aweze kupata huduma. Lazima tusimamie na kuona maeneo yote yanafanya kazi kama ilivyokusudiwa, ili kupata matokeo tarajiwa iwe ni wajibu ya kila mmoja kuhakikisha kuwa anatoa usimamizi thabiti katika eneo lake,” alisisitiza.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na watumishi hao, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Bw. George Simbachawene alisema TAMISEMI wapo tayari kubadilika na kufanya kazi kama kauli ya Rais John Pombe Magufuli inavyotaka, yaani HAPA KAZI TU.

Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Bernard Makali alimpongeza Waziri Mkuu Majaliwa kwa kusimamia vizuri masuala ya elimu nchini wakati akiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya elimu.