Friday , 11th Mar , 2016

Baadhi ya wazee katika mji wa Nanyamba,Mkoani Mtwara wamelalamikia kero za matibabu wanazozipata zinazotokana na kukosekana kwa kituo cha afya cha serikali na kuwalazimu kutumia gharama kubwa katika kituo kinachomilikiwa na shirika la kidini.

Wakizungumza na East Africa Radio, wazee hao wamesema wanapata changamoto katika kupata huduma wanapokwenda katika Zahanati ya Dinyecha kutokana na kukosa utaratibu mzuri wa kuwahudumia wazee na kujikuta wanatumia muda mrefu kupata huduma.

Aidha, wamesema halmashauri hiyo inakabiliwa na kero kubwa ya uhaba wa maji inayotokana na kukosekana kwa umeme katika chanzo cha maji cha Mnyawi, na kupelekea halmashauri kutumia lita 200 kila siku kwa ajili ya mafuta ya kuwasha Jenereta.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Oscar Ng’itu, ameonekana kushangazwa na malalamiko hayo na kudai kuwa aliwahi kutembelea vituo vya afya vyote na Zahanati na kutoa maagizo kwamba kuwe na maeneo maalumu ya kuhudumia wazee, huku akielezea hatua iliyofikiwa katika kutatua kero ya maji.