Saturday , 2nd Aug , 2014

WATU wawili wamefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa vibaya, baada ya basi la kampuni ya Hood kugongana uso kwa uso na daladala, wilayani Arumeru mkoani Arusha.

Kamanda ya Jeshi la Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas

WATU wawili wamefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa vibaya, baada ya basi la kampuni ya Hood lenye namba za usajili T.168 AXM kugongana uso kwa uso na dala dala, iliyokuwa inatoka Usa River, kwenda Jijini Arusha eneo la kilala, wilayani Arumeru jana.

Akizungumzia ajali hiyo mmoja wa mashuda, Ahimidiwe Elias amesema basi hilo la Hood lilikuwa linakimbizana na basi la shabaha, majira ya saa 12:30 asubuhi ya Agosti 2 mwaka huu, ndipo dereva wa Hood alipolipita gari dogo aina ya Subaru na ghafla alikutana na daladala hiyo na kugona uso kwa uso.

Akithibitisha kufariki kwa watu hao Mganga Mkuu wa Hosptali ya Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Dk. Azizi Msuya amesema wamepokea majeruhi 13 na maiti moja ya dereva aliyekuwa akiendesha daladala hiyo.

Dk. Msuya amewataja waliopoteza maisha kuwa ni Jumanne Mohamed aliyekuwa dereva wa daladala hiyo Anaret Sabas aliyefariki dunia akipelekwa katika hosptali ya Mkoa ya Mt Meru kutokana na majeraha makubwa kichwani, yalisababisha damu nyingi kumwagika.

Amewataja majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni pamoja na Renald Gostab na Grace Wilium,Nicholus Laurance na Aminiel Mbise ambo pia walikimbizwa hosptali ya mkoa ya Mt Meru kutokana na majeraha makubwa waliyokuwa nayo kifuani na kichwani na hali zao zilikuwa mbaya sana.

Dk. Msuya amewataja majeruhi wengine ambao wanaendelea na matibabu hosptalini hapo kuwa ni pamoja na Judica Peter, Philopo Kilembi, Kilamba Kiyaganga, Asifiwe Aberi, Witnes Elias, Domic Tusanta Pamoja na Rogathe Kiyungai.

Amesema majeruhi walibakia hosptalini hapo, hali zao zinaendelea vizuri, wanasubiri majibu ya X ray ili kujua kama wapata matatizo kwa ndani, kwa kuwa wengi wao wana majeraha kichwani,kifuani na miguuni.

Dk. Msuya amesema majeruhi wote wa ajali hiyo walikuwa ndani ya daladala hiyo na hakuna abiria yeyote alijeruhiwa katika basi la Hood.

Meneja wa kampuni ya Aziz Msuya, amesema kuwa basi hilo liliondoka standi kuu ya mabasi majira ya saa 12:00 asubuhi kuelekea jijini Mbeya ambapo muda mfupi baadaye alipigiwa simu na dereva wa basi hilo, aliyemtaja kwa jina moja la Omary kuwa wamepata ajali.

Amesema baada ya kupata taarifa hiyo alifanya utaratibu wa kuatafuta basi lingine kwa ajili ya kuwawezesha abiria hao kusafiri na kuwa dereva huyo anashikiliwa na polisi kituo cha Usa River.

Kamanda ya Jeshi la Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas hakuweza kupatikana kuzungumzia tukio hilo, baada ya Afisa habari wa jeshi hilo kusema kuwa kamanda yupo kwenye kikao.