Friday , 30th Sep , 2016

Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Mh. Geoffrey Idelphonce Mwambe amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Bw. Charles Edward Fussi, kuwasimamisha kazi mara moja watumishi watano wa halmashauri hiyo.

Mh. Geoffrey Idelphonce Mwambe

Watumishi hao wametakiwa kusimamishwa ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili na hatua zaidi za kisheria zichukuliwe dhidi yao kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao vizuri, uzembe na utovu wa nidhamu kazini.

Mkuu huyo wa Wilaya amefanya uamuzi huo alipokuwa kwenye mkutano na wafanyakazi wa halmashauri ya wilaya ya Manyoni, ambapo aliwataja watumishi hao alioagiza kusimamishwa kazi kuwa ni Mkuu wa Idara ya Ugavi Bw. Genesius Rugemalira ambaye amesimamishwa kwa kushindwa kusimamia manunuzi ya halmashauri na kuisababishia serikali hasara ya Tshs. Mil 16.

Mwingine ni daktari John Amita wa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni aliyesimamishwa kwa tuhuma za kupigana na daktari mwenzake hospitalini hapo, tuhuma za utoaji mimba, na uzembe uliopelekea kifo cha mama mjamzito.

Wengine waliosimamishwa ni Muuguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni Bw. Mika Iloti kwa uzembe uliopelekea kifo cha mama mjamzimzito, Msaidizi wa Ofisi Bw. Anthony Sanga kwa ufujaji wa mapato ya halmashauri na Mtendaji wa Kijiji cha Makasuku kilichopo Kata ya Sasajila Bw. Mussa Ndahani ambaye kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Kijiji chake wamekuwa wakitoa vibali vya uvunaji misitu kwa wafanyabiashara ya mbao bila kuzingatia sheria na taratibu kwa kofia ya zoezi la utengenezaji wa madawati linaloendelea.

Wakati huo huo Mkuu huyo wa Wilaya ya Manyoni ametoa karipio kali na kumwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kuwachukulia hatua Mganga Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Dkt. Francis Mwanisi kwa kuficha taarifa na kufumbia macho matukio ya utovu wa nidhamu wa madaktari na wauguzi wa hospitali ya wilaya ya Manyoni na Mhasibu Mkuu wa mapato Bw. Elias Mwachinyemba kwa kushirikiana na wazabuni wa ukusanyaji mapato ya halmashauri waliomaliza muda wao kuhujumu mapato ya Halmashauri.

Mh. Mwambe pia ametengua uteuzi wa aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Manyoni, Bw. Yona Chalinze na Kaimu Mhandisi wa Maji Bw. Musoma Kanyere kwa utendaji kazi usioridhisha.

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya ameagiza wakuu wote wa vitengo na Idara za halmashauri mbili anazozisimamia, Halmashauri ya Itigi na Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kumletea taarifa za utendaji wa Idara zao kila ifikapo Tarehe 10 ya mwezi kulingana na mpango kazi ambao idara na vitengo zilikubaliana na Mkuu huyo wa Wilaya wakati wa kuweka mikakati ya Wilaya.

Mwisho, Mkuu huyo wa Wilaya ametoa onyo kali kwa watendaji wote wa vijiji, kata, tarafa, halmashauri na taasisi zote za serikali wilayani Manyoni na kuwataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea bali watimize wajibu wao kwa kuzingatia uadilifu na nidhamu ya kazi ya kuwatumikia wananchi na kuepuka vitendo vya rushwa.