Monday , 20th Oct , 2014

Abiria zaidi ya 45 wengi wao wakiwa ni akina mama na watoto wa familia moja waliokuwa wakienda harusini, wamenusurika kifo baada ya basi dogo la abiria aina ya coaster la kampuni ya ''Slim'' kushindwa kupanda mlima mkoani Tanga

Abiria zaidi ya 45 wengi wao wakiwa ni akina mama na watoto wa familia moja waliokuwa wakienda harusini, wamenusurika kifo baada ya basi dogo la abiria aina ya coaster la kampuni ya ''Slim'' kushindwa kupanda mlima wa kutoka tarafa ya Soni kwenda jimbo la bumbuli wilayani lushoto na kusababisha gari hilo kurudi nyuma kisha kwenda kugonga gema la barabara na kusimama.

Wakizungumza na EATV katika eneo la tukio katikati ya mlima Soni wenye bonde kubwa lenye urefu wa mita zaidi ya 100 kwenda chini, baadhi ya waathirika wa tukio hilo wameliomba jeshi la polisi kufanya ukaguzi wa mabasi yanayofanya safari zake kutoka Tanga kwenda katika maeneo yenye miinuko kwa sababu kama lingerudi nyuma na kwenda kutumbukia katika bonde lililopo pembeni mwa barabara hiyo hakuna abiria hata mmoja ambaye angenusurika.
 
Kwa upande wao dereva na kondakta wa basi hilo linalofanya safari zake kutoka jijini Tanga kwenda jimbo la Bumbuli wamesema ilitumika akili ya ziada kusaidia kuokoa maisha ya abiria hao kwa sababu dereva alijaribu kuweka gia namba moja lakini ilikataa ndipo alipoamua kukata kona kali ili gari hilo liweze kwenda kulia kwake kwa lengo la kwenda kugonga gema la barabara hiyo ili liweze kusimama.
 
Kufuatia hatua hiyo mkuu wa wilaya ya Lushoto Majid Mwanga amewaagiza wamiliki wa vyombo vya usafiri wa magari ya abiria kuhakikisha kuwa wanayafanyia ukaguzi magari yao kabla ya kusafiri kwa sababu jiografia ya wilaya ya Lushoto imezungukwa na milima na mabonde hatua ambayo ni hatari kwa vyombo vya usafiri ambavyo ni vibovu.