Wednesday , 14th Oct , 2015

Misa maalum ya kumwombea baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefariki dunia Oktoba 14 mwaka 1999 imefanyika leo mkoani Dodoma ambapo katika ibada hiyo watanzania wamehimizwa kushiriki katika uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu.

Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere

Akihubiri katika misa hiyo iliyofanyika leo katika uwanja wa mwalimu Nyerere Makamu wa askofu mkuu jimbo kuu katoliki Dodoma, Chesco Msaga, amewataka watanzania kushiriki uchaguzi mkuu na kuwachagua viongozi wanaowataka kwa utulivu na amani kwa kufuata misingi aliyoiacha baba wa taifa mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Makamu huyo wa askofu amesema kuwa watanzania hawana budi kuishi kutokana na misingi aliyoicha Mwalimu Nyerere ambayo ni amani na mshikamano kwani ndiyo tunu kubwa kwa taifa letu.

Amesema kuwa katika kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu watanzania wanatakiwa kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua kiongozi wanayemtaka bila kuharibu amani na mshikamano aliouenzi baba wa taifa wakati wa uhai wake.

“Tusiharibu kabisa misingi aliyoweka baba wa taifa kwa kutaka madaraka kwa fujo au kufanya fujo ili kuweza kujipatia sifa za kisiasa hivyo basi niwasihi kuhakikisha amani utulivu na mashikano aliyoiweka baba wa taifa tunailinda katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa kushiriki katika kupiga kura bila ya kumbuguzi mtu” alisema Msaga.

Aidha amesema kuwa watanzania wanatakiwa kuiga mambo mengi aliyokuwa akiyafanya baba wa taifa ikiwa ni pamoja na kutokuwa na tabia ya kujilimbikizia mali kama ilivyo kwa baadhi ya watu.

Naye mkuu wa mkoa wa Dodoma Chiku Gallawa, akitoa salamu za mkoa katika ibada hiyo amesema kuwa watanzania wataendelea kumkumbuka Baba wa taifa kwa mambo mengi ambayo aliyafanya wakati wa uhai wake kwa kuwafanya wawe wamoja.

Katika ibada hiyo viongozi wengine walioshiriki ni Spika wa bunge Anna Makinda, Waziri wa habari utamaduni na Michezo Fenela Mukangara, Katibu Mkuu Tamisemi Jumanne Sagini pamoja na makatibu tawala na wakuu wa wilaya mbalimbali.