Wednesday , 19th Aug , 2015

Watanzania wametakiwa kujenga utamaduni wa kupenda kutembelea hifadhi za Taifa (TANAPA) ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya kuhamasisha watanzania kuweza kutembelea hifadhi za taifa yenye kaulimbiu isemayo tembelea hifadhi za taifa ufaidike.

Baadhi ya Wanyama wanaopatika katika mbuga zilizochini ya Hifadhi ya Taifa TANAPA

Hayo yamesemwa na Victor Raphael Kintansi ambaye ni kaimu meneja masoko wa hifadhi ya taifa (TANAPA)wakati akizungumza na waandishi wa habari na wadau wa utalii katika press conference iliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Tanga Beach Resort iliyopo eneo la Sahare jijini Tanga.

Bw, Victor amesema lengo la kampeni hiyo ni kupata watalii wa ndani wapatao laki tano kwa mwaka huu kama ongezeko la watalii wa ndani tofauti na miaka mingine iliyopita.

Aidha ameongeza kuwa zipo zawadi mbalimbali zinazotolewa kwa watanzania wanaotembelea hifadhi mbalimbali za taifa mara baada ya watalii hao kutembelea hifadhi yoyote kwa zaidi ya mara moja.

Sambamba na hayo ameeleza kuwa mtalii wa ndani atakayeweza kutembelea hifadhi yoyote zaidi ya mara nne kipindi hiki cha kampeni atapata zawadi ya juu kutoka shirika la hifadhi za Taifa TANAPA ya kumpeleka mtanzania katika hifadhi ya taifa ya Serengeti au Gombe na kulala kwenye hoteli yenye hadhi ya nyota tano kwa gharama za TANAPA.

Kwa upande wake Pellagy R. Marandu ambaye ni Afisa Utalii mwandamizi kutoka hifadhi ya taifa ya Mkomazi amesema watanzania wengi wameonekana kuwa bado hawajaelewa umuhimu wa kutembelea vivutio vingi kwakuhofia kuwa gharama ni kubwa huku akiwatoa hofu watanzania kuwa gharama zao zinatofautioana na watalii wa nje.