Akieleza matukio hayo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishina Msaidizi wa jeshi la Polisi bwana Thobias Sedoyeka, amesema tukio la kwanza watu wawili wamezama katika bwawa lililoko katika kijiji cha Agondi wilayani Manyoni wakati wakiogelea, tukio lingine mwanafunzi aliye maliza darasa la Saba, ambaye alikuwa amepanda baiskeli amegongwa na gari la mizigo katika kijiji cha kibigiri wilayani Iramba kwenye barabara kuu itokayo Singida kuelekea mwanza.
ACP Sedoyeka amesema tukio la mwisho ni watu wawili wamefariki katika kijiji cha mwamatiga wilayani Manyoni baada ya Bwana Bhija Jandika kumchoma kisu Bwana Shija Masele katika kilabu cha pombe na hatimaye watu wenye hasira kuamua kujichukulia sheria mkononi na kumpiga Bwana Shija Masele kwa mawe na magongo na kusababisha kifo chake.
Kwa upande wao waokoaji na mashuhuda waliofika kutoa msaada wamesema pamoja na kwamba bwawa hilo limekuwa msaada mkubwa katika kijiji chao kwa kuchota maji kwa ajili ya matumizi ya kawaida pamoja na mifugo kunywa ,imefika wakati sasa wazazi kuwaelimisha vijana wao kuacha kuogelea katika bwawa hilo ,ni hatari kwasababu lina kina kirefu pia lina mawe yenye incha kali.
Bwawa la Aghondi ambalo lina hudumia wananchi zaidi ya watu Elfu Mbili wa vijiji viwili vya Aghondi na kaminyanga wilayani Manyoni, lina chemchem ambayo inatoa maji chini ya ardhi na mazuri kwa ajili ya matumizi ya binadamu na mifugo , bwawa hilo limetokea baada ya mkandaras wa kampuni ya CGC iliyokuwa ikijenga barabara kuu ya lami kutoka Manyoni hadi Singida kuchimba kokoto sehemu hiyo.