Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu, Balozi Ombeni Sefue.
Kauli hiyo imetolewa jana na Katibu mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue kwenye kongamano la tano la Kitaifa la makatibu Mahususi na mkutano mkuu watatu wa mwaka uliofanyika kwenye ukumbi wa Chimwaga mjini Dodoma.
Sefue amesema kuwa serikali itafungua namba maalum ya simu kwa ajili ya makatibu Mahususi nchini kuitumia pale wanapofanyiwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia ambavyo vimeonekana kushamiri katika ofisi nyingi za umma na hata zile za watu binafsi.
Amesema kuwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia ni tabia ambayo haikubaliki na ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imeonekana kushika kasi kutokana na makatibu hao kutokuwa na sehemu ya kusemea.
Aidha amewataka makatibu mahususi hao kuwa waaminifu na watu wenye kutunza siri za kazi zao kwani bila ya kufanya hivyo wanaweza kupoteza ajira zao bila kutegemea.
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa chama cha makatibu mahususi nchini (TAPSEA) Janejelly James ameiomba serikali kuitambua taaluma ya makatibu mahususi kwani imevamiwa na watu ambao wanaharibu sifa ya taaluma hiyo.