Thursday , 1st May , 2014

Mamlaka ya usafiri na majini nchini Tanzania Sumatra, kanda ya mashariki, imesema kuwa kuanzia sasa madereva wa vyombo vyote vinavyokiuka taratibu za usafiri watafikishwa katika vyombo vya dola kwa hatua zaidi za kisheria.

Afisa Mfawidhi wa sumatra kanda ya mashariki, Conrad Shio, akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa habari. Kulia kwake ni mkuu wa kikosi cha usalama barabarani, Kamanda Mohammed Mpinga.

Afisa Mfawidhi wa Sumatra kanda ya mashariki Conrad Shio ametaja baadhi ya makosa ambayo yamepewa kipaumbele kwa sasa kuwa ni uingiaji wa pikipiki na bajaji katika maeneo ya katikati ya jiji la Dar es Salaam pamoja na makosa yanayofanywa na vyombo vya usafiri wa umma ikiwa ni pamoja na kufanya kazi pasipo kusajiliwa.

Shio amesema makosa hayo pamoja na mengine yana vifungu vya sheria vinavyoruhusu mamlaka nyingine za serikali kuingilia kati ikiwa ni pamoja na kulipa faini sambamba na watuhumiwa kufikishwa mahakamani.