Sunday , 20th Jul , 2014

Wajumbe wa Kikundi Kazi cha Serikali za Mitaa cha Policy Forum, wamependekeza uchaguzi wa serikali za mitaa ufanyike mwakani pamoja na uchaguzi mkuu kama ilivyofanya Kenya na Zimbabwe.

Hebron Mwakagenda, Mwenyekiti wa Kikundi Kazi cha Serikali za Mitaa cha Policy Forum.

Mwenyekiti wa Kikundi hicho ambacho kinawakilisha zaidi ya asasi za kiraia 70, Hebron Mwakagenda, ametoa kauli hiyo katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam hapo jana.

Katika mkutano huo, Mwakagenda amesema wanamuunga mkono Rais Jakaya Kikwete kuwa taifa lipo kwenye mtikisiko kuhusiana wa mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya.

Amesema wanatambua Tamisemi siyo chombo mahususi cha kuendesha chaguzi nchini hivyo wamependekeza uchaguzi wa serikali za mitaa usimamiwe na kuendeshwa na Tume Huru ya Uchaguzi na kwa sasa wapate nafasi ya kubadilisha sheria za uchaguzi na kufanya maandalizi mengine ili uchaguzi uwe huru.

Amesema kutokana na umuhimu wa uchaguzi huo, wameamua kutoa mchango wao katika mchakato huo na kufafanua kuwa serikali za mitaa zinalenga kupeleka au kuyasogeza madaraka kwa jamii ili kufanya maamuzi, kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma kulingana na matakwa ya wananchi.

“Mchakato wa uchaguzi huu unategemea mchakato wa katiba mpya ambao umepoteza ratiba yake ya awali kwa kuwa ingetakiwa kuzinduliwa Aprili 26, mwaka huu lakini upo njia panda,” alisema na kuongeza:

Mwakagenda alisema wanapenda kufahamu uchaguzi huo utafanyika lini kwa kuwa kwa kawaida kipindi kama hiki kanuni za uchaguzi huwa zimeshaandaliwa na kutolewa.