Wapagazi wakiwa wanawasindikiza watalii kupanda Mlima Kilimanjaro.
Hatua hiyo imechukuliwa ikiwa ni mkakati mahususi wa kuondoa athari zinazowakumba wapagazi wapatao elfu kumi na saba na mia nane waliosajiliwa,ambao wanabeba mizigo ya watalii wanaopanda milima hiyo kutokana na baadhi yao kupoteza maisha kwa kushindwa kumudu gharama za matibabu pindi wanapougua wakiwa ndani ama nje ya eneo la kazi.
Wakitoa maelekezo kwa wajumbe wa chama cha wapagazi kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro juu ya utaratibu huo mpya, Viongozi wa Chama hicho akiwemo Mwenyekiti wake wa Bodi Alex Lemunge,wamesema inawalazimu kuunda utaratibu huo ili kuwakinga na athari za vifo vinavyotokana na ukosefu wa fedha za matibabu kwa watu wanaofanya kazi ngumu za kupandisha mizigo ya watalii kwenye milima hiyo miwili..
Wakati azimio hilo likipitishwa tayari Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya imeendelea na zoezi lake la kutoa elimu kwa vikundi vyenye mrengo wa kiuchumi kuhusu manufaa yanayopatikana kupitia mifuko hiyo.
Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoa wa Arusha,Anisya Ngweshemi akizungumza na Wapagazi kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, amesema ni wakati muafaka sasa kwa watu kutoka sekta binafsi kutumia fursa ya kufunguliwa milango ya makampuni binafsi kuingia katika mifuko ya Bima ya Afya inayotoa huduma zake kuanzia kwenye vituo vya Afya hadi hospitali za Rufaa nchini kote...
Inaelezwa kwamba kutokuwepo kwa mikataba iliyo rasmi baina ya wapagazi na makampuni ya utalii kunachangia kwa kiasi kikubwa makampuni mengi kukwepa jukumu la kuwahudumia wapagazi na huwenda hatua ya kujiunga kwao na mifuko ya Bima ya Afya kukamwondolea mhusika mzigo wa kujihudumia pindi anapougua.