Monday , 12th Oct , 2015

Watu wanne wamejruhiwa katika matukio mawili tofauti yanayohusishwa na vurugu za kiasiasa katika mikoa ya Mtwara na Dar es Salaam ikiwemo wawili waliolazwa baada ya kukatwa mapanga baada ya kutoka katika Mkutano wa Kampeni.

Wanachama wa Chama cha Mapinduzi wakiwa katika moja ya Mikutano ya kampeni ya Chama hicho.

Katika tukio la Kwanza Jijini Dar es Salaam wanachama wawili wa CCM inadaiwa walivamiwa na wafuasi wanaodhaniwa ni wanaounga mkono UKAWA na kukatwa mapanga eneo la Sinza katika Manispaa ya Kinondoni hatua ambayo imekemewa na baadhi ya viongozi wa chama hicho na kuomba vyombo vya sheria kuingilia kati huku majeruhiwa wa tukio hilo akilezea jinsi ya walivyovamiwa na watu hao.

Katika tukio jingine wanachama wawili wa Chama cha Wananchi (CUF) manispaa ya Mtwara Mikindani, Kisa Mwaya na Haji Bakari, wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya Ligula, huku wakiugulia maumivu waliyoyapata baada ya kutekwa na kupewa kipigo na watu wasiojulikana usiku wa Oktoba 9 kuamkia juzi Oktoba 10 mwaka huu.

Wakizungumza leo hospitalini hapo, wamesema mazingira yakutekwa kwao yanafanana kwasababu wote walitekwa siku moja ambapo ilikuwa ni usiku huku kila mtu akifuatwa nyumbani kwake na watu ambao walijifanya ni askari.

Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Mhuza Mdoe amekiri kuwapokea wanachama hao, lakini hakutaka kuzungumzia hali zao na namna walivyoathirika ndani ya miili yao.

Naye, mkurugenzi wa siasa wa CUF mkoa wa Mtwara, Saidi Mtunduima, amesema bado chama hakijafanya uchunguzi wowote juu ya tukio hilo huku wakisubiri wenyewe wapate nafuu na kuweza kueleza vizuri pengine watawakumbuka waliowafanyia kitendo hicho.

Kamanda wa polisi mkoani humo, Henry Mwaibambe, alipoulizwa juu ya tukio hilo, alisema halijui kwasababu bado halijafika ofisini kwake, hivyo hawezi kuzungumza lolote.

Tukio hilo linakuja wiki moja baada ya kutokea tukio la kutekwa na kuteswa kwa mgombea ubunge wa jimbo la Mtwara mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Joel Nanauka, ambaye hata hivyo watu waliofanya hivyo bado hawajafahamika.