Wednesday , 8th Mar , 2017

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angela Kairuki ameungana na wafanyakazi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya hospitali hiyo kwa lengo la kuadhimisha Siku ya Wanawake duniani.

Mh. Angela Kairuki akiongoza Wanawake wenzake wa CCM mkoa wa dar es Salaam kutoa msaada katika Hospitali ya Taifa Muhimbili

Mhe. Kairuki ambaye pia ni Mbunge wa viti maalum kupitia CCM amesema katika kusherekea siku hii umoja wa wanawake wa chama cha Mapinduzi (UWT) wameona ni vema wakashiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii ili kuonesha dhamira ya dhati kwamba wanamthamini mwanamke.

“Sisi tumekuja hapa Muhimbili kushiriki na ninyi katika kuadhimisha siku hii kwa kufanya usafi bila kujali itikadi ya chama kwani Hospitali hii inahudumia wananchi wote , pia siku hii ya leo tunatoa msaada wa vitanda 10  pamoja na mashuka yake pia wenzetu wengine wameenda katika hospitali nyingine wote tukiwa na lengo moja’’.  Amesema Kairuki

Hata hivyo Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga wa MNH Bi. Agnes Mtawa amewashukuru UWT kwa msaada walioutoa katika hospitali hiyo huku akiwakumbusha wauguzi kuendelea kufanya kazi kwa ueledi uliotukuka kwani kazi hiyo inahitaji moyo wa huruma na kujitoa zaidi.