Saturday , 2nd Jul , 2016

Rushwa ya ngono imetajwa kusababisha vifo, magonjwa, kuzalisha wataalamu wa bovu na kuongeza utendaji kazi duni miongoni mwa taasisi mbalimbali nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambaye pia ni mwenyekiti wa umoja wa kupambana na rushwa ya ngono vyuoni Dkt. Colman Msoka katika mkutano na taasisi ya jinsia na taasisi ya wanawake Tanzania, ambapo ameitaka jamii kuachana na vitendo hivyo ambavyo vinalenga udhalilishaji na kuondoa utu wa mtu.

Aidha Dkt Msoka, amesema rushwa hiyo imekuwa kichocheo cha nidhamu mbovu, mifarakano miongoni mwa wanafunzi, waalimu na makundi mengine katika jamii na baadaye kupeleka vifo hali ambayo amewataka wapenda haki kutofumbia macho uombaji na utoaji wa rushwa ya ngono hasa maeneo ya vyuoni.

Ameongeza kuwa kushamiri kwa suala hilo kunatokana na imani iliyojengeka miongoni mwa watu ya kutaka kupata mafanikio kwa njia rahisi jambo ambalo Dkt Msoka amewataka wasomi hasa wa vyuo vikuu kutumia juhudi na ufanisi binafsi kupata ajira na kutatua changamoto mbalimbali.