Thursday , 9th Jul , 2015

Wananchi na wakulima wa zao la korosho wametakiwa kula kwa wingi zao hilo ili kuimarisha afya zao na kukuza soko la ndani litakalopelekea kukua kwa uchumi wa taifa.

Zao la Korosho likiwa shambani ambalo linatumika kwa shughuli tofauti tofauti.

Akizungumza na East Africa Radio, Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Mfaume Juma, amesema zao hilo lina faida nyingi kwa binadamu ambazo sio za kubuni na kwamba hata nchi zilizopiga hatua katika uuzaji wa korosho zilizo banguliwa ambazo ni Vietinam na India, zinatangaza manufaa yake katika soko la kimataifa.

Mfaume amesema kuwa Korosho ina umuhimu mkubwa kwa watoto, akina mama wajawazito pamoja na watu wenye afya zilizodhoofu na kuboresha afya hivyo zao la korosho lichukuliwe kama dawa.

Kwa upande wake, katibu mtendaji wa mfuko wa Kuendeleza zao la Korosho (WAKFU) Suleiman Lenga, amesema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaboresha ubanguaji wa zao hilo ambapo kwa sasa wameshapata maeneo matatu kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vitatu vya ubanguaji.