Friday , 22nd Apr , 2016

Kampuni ya Unique Consultant Company Limited (UCC) inayofanya kazi ya kuajiri watu katika kiwanda cha Saruji cha Dangote Industry Limited mkoani Mtwara, imelalamikiwa na wananchi kutoa ajira kwa ubaguzi na kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa

Muonekano wa baadhi ya Majengo ya Kiwanda cha Dangote

Wakizungumza katika kikako cha ujirani mwema kilichoitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, ambaye aliwaita viongozi wa kiwanda hicho kwa ajili ya kujibu hoja za wananchi, wamesema vijana wengi wanaoishi katika vijiji jirani na kiwanda hicho wananyimwa fursa za kuajiriwa kwa kigezo cha kutojua lugha ya Kiingereza.

Wamesema wataalamu wengi katika vitengo mbalimbali kiwandani hapo ikiwa ni pamoja na wahandisi, ni raia wa Kichina ambao awali walikuwa wanajua lugha ya Kichina pekee, hivyo wamejifunza lugha za Kiingereza na Kiswahili wakiwa kazini jambo ambalo linaweza kufanyika pia kwa wakazi wa maeneo hayo.

Akijibu hoja hizo, Mwanasheria wa Kampuni hiyo, Robert Makwaia amesema suala la kigezo cha lugha ni sehemu tu ya vigezo vinavyohitajika na kwamba vipo vingine vingi vinavyohitajika ambapo hata hivyo hakuweka wazi vigezo hivyo, huku akikanusha tuhuma za rushwa na kudai kuwa mtoa hoja inawezekana ametunga tu katika kikao hicho.

Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, amekiri kupokea malalamiko kutoka kwa miongoni mwa wananchi juu ya kuwapo kwa vitendo vya rushwa kiwandani hapo na kudai kuwa vitendo hivyo vipo pia katika ngazi za Vijiji, Kata hadi Tarafa.