Tuesday , 23rd Feb , 2016

Wananchi Wilayani Newala wamelalamikia ukosefu wa dawa katika vituo vya afya na Zahanati na kudai kuwa hali hiyo inachangia watu wengi kutoona haja ya kujiunga katika Mfuko ya Afya ya Jamii (CHF).

Mkuu wa Wilaya ya Newala Mkoani Mtwara, Christopher Magala akifungua mkutano wa wananchi.

Wakizungumza katika uzinduzi wa kitaifa wa uhamasishaji wa mfuko wa afya ya jamii CHF mkoa wa Mtwara, uliofanyika katika kata za Kitangali na Chiwonga wilayani humo, wananchi hao wamesema hali hiyo inawavunja moyo wananchi ambao wengi wao wana kipato cha kawaida.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Newala, Christopher Magala,ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, amewataka wananchi wa kata hizo, kuona umuhimu wa kijiunga na mfuko huo na kuwasisitiza kuwa ugonjwa unapoingia mwilini kwa mtu hauwezi kubisha hodi.

Naye, mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Newala, Maimuna Mtanda, amesema lengo la mfuko huo ni kuwafanya wananchi wachangie huduma ya afya na sio lazima watoe michango yao kwa mkupuo bali wanaweza kuchangia kwa awamu.